Madaktari Bingwa wa Saratani na wataalamu mbalimbali wa matibabu ya ugonjwa huo, wamekutana Jijini Dar es Salaam, Katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa kujadili maendeleo na hatua zaidi ya kudhibiti ugonjwa huo tishio duniani.
Akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa Chama Cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania, Jerry Ndumbaro, amesema unalengo la kujadili maendeleo ya matibabu ya Saratani na matokeo ya tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika.
Pia, alipomgeza jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kudhibiti ugonjwa wa saratani ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kisasa itawezesha idadi ya vifo na wagonjwa wa saratani kupungua kwa kasi katika miaka 10 ijayo.
Aliyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam, kupitia Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wataalamu wa Saratani, uliowakutanisha madaktari bingwa wa saratani wa ndani na nje ya nchi, ambapo alisema kwasasa wagonjwa wengi wanagundua saratabi katika hatua za awali hali inayosaidia kuokoa maisha yao.
“Katika saratani ya shingo ya kizazi, kwa sasa serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa ambapo kuna vituo vya kupima dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi, karibu hospitali zote nchini kuanzia ngazi ya vituo vya afya na zile kubwa, hivyo watu wanapata fursa ya kupima bure.
“Katika miaka michache tangua kuanza kutolewa huduma hiyo na kuwapa watu fursa ya kupima wagonjwa wengi katika hatua za awali, imeonesha kuwa wagonjwa wengi wamegundua ugonjwa huo katika hatua za awali tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo wengi walifika wakiwa hatuaya tatu na nne, ambayo ni hatari zaidi,”amesema.
Amesema katika kinga, kwa sasa serikali inatoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, kwa wasichana wenye umri kati ya miaka tisa hadi 14, ambapo kwa takwimu za wizara ya afya zinaonesha asilimia 84 hadi 90 wamepata chanjo hiyo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Saratani, Emmanuel Mduma, alisema mkutano huo wa nne wa kimataifa wa saratani kufanyika nchini unatija kubwa katika maendeleo ya tafiti, kusaidia katika kutoa tiba stahiki kwa wagonjwa wa saratani.
Alisema changamoto kubwa ambayo bado ipo ni magonjwa kufika hospitalini kwa kuchelewa hali inayosababisha kupata changamoto kubwa, tofauti na vile ambavyo wangefika katika hatua za awali wangepata tiba vizuri.
Katika hatua nyingine, Daktari Bingwa, Ratifa Abdallah, alisema mkutano huo umekuwa na tija kubwa katika kujadili maendeleo ya matibabu ya kisasa kupitia radiolojia kupitia matundu madogo ikiwa ni hatua kubwa ya matibabu ya saratani.
Alifafanua kuwa, matibabu ya tundu dogo yamesaidia kwa hatua kubwa kumtibia mgonjwa kwa njia hiyo ya kisasa , hali inayosaidia kwa hatua kubwa kurahisisha matibabu kuepusha upotevu wa damu nyingi, tofauti na vile ambavyo mgonjwa angepasuliwa.


Post a Comment