MSIMAMO WA TRA KUTOFUNGIA BIASHARA UMEZINGATIA MASLAHI YA PANDE ZOTE

..........

NA: DK. REUBENI LUMBAGALA 

Kuna mabadiliko makubwa ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa namna wanavyoendesha shughuli zao. Mabadiliko hayo yamezingatia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji kodi bila kuumiza upande mwingine.

TRA katika kutimiza wajibu wake wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara na walipakodi wengine, wamebadili utaratibu wao wa awali ambao ulihusisha kufungia biashara kwa mfanyabiashara aliyeshindwa kulipa kodi kwa wakati.

Jambo hili lilikuwa likilalamikiwa na walipakodi wengi kwani kufungia biashara kuliwaua kiuchumi wafanyabiashara na kufifisha matumaini ya kulipa kodi wanayodaiwa na TRA, hivyo serikali kukosa mapato yake. Kiufupi, utaratibu huu ulikuwa msiba mkubwa wa kiuchumi na maendeleo.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika maelekezo yake kwa TRA, alipiga marufuku matumizi ya vikosi kazi katika ukusanyaji kodi na kufungia biashara. Maelekezo hayo yakapokelewa vyema na TRA wakiongozwa na Kamishna Mkuu wake, CPA Yusuph Mwenda.

Sasa ni faraja kuona kuwa, kwa mlipakodi anayedaiwa kodi anaweza kuendelea na biashara yake huku akilipa kidogo kidogo deni lake. Utaratibu huu ni mzuri kwani unampa fursa mfanyabiashara kuendelea kuingiza kipato kwa ajili ya kukuza biashara yake na kujipatia mahitaji muhimu kwa ajili ya maisha yake huku serikali ikiwa na uhakika wa kupata kodi yake.

Kamishna Mkuu, CPA Mwenda, akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Oktoba 19, 2026, aliendelea kusisitiza kuwa hakuna biashara yeyote itakayofungwa kwa sababu ya kodi, kwani TRA ina wajibu wa kukuza biashara za wateja wake.

CPA Mwenda aliwahakikishia wafanyabiashara wa Kilombero kuwa TRA ipo pamoja nao katika kuwapatia elimu ya ulipajikodi ili malengo ya serikali yaweze kufanikiwa.

"Niwahakikishie wafanyabiashara kuwa hakuna biashara yeyote itakayofungwa kwa sababu mfanyabiashara ameshindwa kulipa kodi, mfanyabiashara ataendelea kufanya biashara huku akilipa kodi," amesema CPA Mwenda.

Kwa hakika, utaratibu huu unaakisi dhamira ya serikali ya kutumia utu katika utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, maamuzi haya yamezingatia maslahi ya pande zote, yaani serikali ikusanye mapato yake huku mfanyabiashara naye akiendelea kufanya shughuli zake kwa amani.
 

0/Post a Comment/Comments