Na MwandishI wetu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande (Mb) amezindua Kituo cha Wageni cha Serengeti kilichopo ndani ya hifadhi hiyo kitakachosaidia katika utoaji wa taarifa kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali Duniani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri Chande amebainisha kuwa uwepo wa kituo hicho ni hatua muhimu na mahsusi ya kukutanisha wageni na wanaothamini mazingira ya asili na uhifadhi wa wanyamapori waliopo kwenye eneo hilo kwa ajili ya kujifunza na kufanya tafiti katika kubaini siri za ikolojia.
Chande amesema uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni alama muhimu kwa Tanzania na Duniani kwa ujumla ikijivunia kuwa hifadhi ya uhalisia wa ikolojia ya kipekee ya uhifadhi wa wanyamapori huku ikiendelea kuwa alama muhimu yenye hadhi ya Kimataifa.
"Kwa ujumla ujenzi wa kituo hiki na uzinduzi wake utaleta ufanisi mkubwa kwa wageni wanaokuja kutembelea Hifadhi yetu ya Serengeti kwa sababu wageni watapata taarifa muhimu kabla hawajakwenda kujionea utajiri wa vivutio tulivyonavyo," alisema Mhe. Chande.
Amesema kupitia maonesho yaliyopo kwenye kituo hicho, kituo kitaweza kuwaalika wageni mbalimbali ikiwemo wanafunzi na watafiti mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kujifunza na kuelewa kuwa kutunza maeneo ya hifadhi ni wajibu na jukumu la pamoja katika kutunza utajiri na urithi wa Tanzania kwa kizazi hiki na kijacho











Post a Comment