.....
Na Carlos Claudio, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni utekelezaji wa maono ya muda mrefu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyependekeza kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma mwaka 1983.
Akizungumza leo, Oktoba 30, 2026, jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, Rais Samia amesema uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ulizingatia nafasi yake ya kijiografia, ikiwa katikati ya nchi na kuwa karibu na wananchi kutoka mikoa mbalimbali.
Amesema maono hayo yaliendelezwa na marais waliomtangulia, akiwemo Hayati Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambao kila mmoja alichangia katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa azma hiyo.
Aidha, ametoa shukrani za pekee kwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa mwaka 2016 wa kuhamishia shughuli za Serikali jijini Dodoma, hatua aliyoieleza kuwa ilichochea utekelezaji wa vitendo wa maono ya Baba wa Taifa.
Rais Samia amesema Aprili 13, 2019, Hayati Dkt. Magufuli alizindua Mji wa Serikali Mtumba baada ya kukamilika kwa majengo ya awali ya muda yaliyowezesha wizara, ofisi na taasisi mbalimbali za Serikali kuanza kutoa huduma katika eneo hilo, ambalo wakati huo lilipewa jina la Magufuli City.
Ameeleza kuwa baada ya kukabidhiwa dhamana ya kuliongoza taifa mwaka 2021, Serikali yake iliendelea na kazi ya kuendeleza mji huo kwa kujenga majengo ya kudumu ya ghorofa, barabara za lami pamoja na miundombinu mingine muhimu na wezeshi ili kukamilisha azma iliyowekwa.
Katika hafla hiyo, Rais Samia amesema mafanikio yaliyofikiwa ni matokeo ya usimamizi na ushirikiano wa viongozi pamoja na watendaji wa Serikali walioshiriki katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo, huku akiwapongeza Watanzania kwa mafanikio hayo.
Uzinduzi huo umehusisha majengo 26 ya wizara, majengo 11 ya taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 59.1 na miundombinu mingine iliyojengwa katika eneo hilo.
Kukamilika kwa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha shughuli za kiutawala jijini Dodoma, kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuboresha uratibu wa shughuli za Serikali na kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi za umma.
Vilevile, uwepo wa Mji wa Serikali Mtumba unatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii jijini Dodoma kupitia kukuza shughuli za biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Rais Samia amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kuwa na makao makuu ya Serikali yenye miundombinu ya kisasa, yanayokidhi mahitaji ya kiutawala na kutoa mazingira bora ya utendaji kazi.


Post a Comment