RIZIKI MVUNGI: PROGRAMU YA BARRICK YA KUANDAA KIZAZI KIPYA CHA WATAALAMU WA SEKTA YA MADINI NI FURSA KWA WANAWAKE KUINGIA KATIKA TASNIA

Riziki Mvungi akipokea nyaraka za ufadhili wa kwenda kusoma shahada ya kwanza ya sayansi ya Jiolojia na Madini katika Chuo Kikuu cha Johannesburg Afrika ya Kusini kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, wa kwanza kushoto ni Meneja wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido na mwanzo kulia , Mkuu wa Shule ya Madini na Sayansi ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOMG), Profesa Elisante Mshiu (picha kutoka maktaba).

***
Katika kufanikisha mkakati wa kusuka kizazi kipya cha wataalamu wa sekta ya madini sambamba na kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika tasnia ya madini, Barrick inatekeleza program katika kanda ya Afrika na Afrika Mashariki ya kuwezesha wasomi vijana kupata ufadhili wa kusomea fani ya madini katika vyuo vikuu vya nje ya nchi watokazo.

Katika awamu ya kwanza ya program hii katika mchujo uliofanyika mapema mwaka huu, vijana watano kutoka Tanzania walishinda ufadhili wa program hiyo kwa sasa wapo wanaendelea na masomo ya tasnia ya madini katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.

Ufadhili huo wa Barrick Tanzania unawezesha wanufaika kulipiwa gharama zote katika kipindi cha masomo ikiwemo kupatiwa fursa ya kufanya masomo ya vitendo katika migodi ya Barrick nchini ya North Mara uliopo mkoani Mara na Bulyanhulu uliopo mkoani Shinyanga.

Riziki Mvungi ni binti wa Kitanzania na mmoja ya wanafunzi watano wa mwaka wa kwanza kutoka Shule ya Madini na Sayansi ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOMG) aliyeshinda nafasi ya ufadhili huo.

Katika mahojiano karibuni kuhusiana anavyoichukulia fursa hiyo aliyoipata, Riziki alisema anajivunia kuipata kwa kuwa ilikuwa na ushindani mkubwa na anaona kampuni ya Barrick nchini Tanzania itafanikisha kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasayansi aliyebobea katika katika fani ya uhandisi wa Madini, fani ya ndoto yake ambayo anasomea kwa sasa.

“Ufadhili huu nilioupata kutoka Barrick sio wa kifedha tu bali kwangu ni njia ya kunijenga kuwa mtaalamu wa kitanzania wa fani ya madini na natumia fursa hii kusoma kwa bidii ili niweze kumaliza masomo yangu nikiwa na utaalamu unaotakiwa kufanya kazi mhandisi wa madini wa kisasa mwenye viwango vya kimataifa”, alisema Riziki.

Pia Riziki anasema kuwa kusomea katika chuo Kikuu kikubwa cha Johannesburg na kufanya masomo ya vitendo katika migodi ya Barrick kumezidi kumjenga kitaaluma, kumwongezea kujiamini zaidi na kumuandaa kuingia katika Tasnia ya madini akiwa ni mtaalamu.

“Kufanya masomo ya vitendo kwenye Migodi ya Barrick nchini kumeniwezesha kukutana na wataalamu wa kunifundisha masuala mbalimbali ya madini waliobobea katika fani pia kampuni imewekeza kwenye matumizi ya teknojia za kisasa kwendana na mafunzo tunayoendelea kuyapata darasani ikiwemo mambo mengine mapya kuhusiana na fani ya madini”,alisema Riziki.

Alipoulizwa anatoa ushauri gani kwa wanawake kuingia katika tasnia ya madini ambayo kwa muda mrefu imetawaliwa na wanaume,Riziki alisema kuwa kinachotakiwa ni wanawake kujiamini, kusoma kwa bidii masomo ya kuwawezesha kusomea fani ya madini na kujifunza ujuzi unaotakiwa migodini .

Pia Riziki alisema kuwa wanawake wakijengewa mazingira mazuri ya kufanya kazi migodini na kupatiwa mafunzo kwa vitendo ana uhakika idadi ya wanawake itaongezeka na sio kwa wafanyakazi tu bali wanaofanya biashara na migodi,kinachotakiwa ni kujiamini na kuwa tayari kujifunza mambo mbalimbali yaliyopo kwenye tasnia ambayo yanabadilika kwa kasi siku hadi siku.

Alitoa wito kwa wasichana waliopo mashuleni wachangamkie masomo ya sayansi ili wapate nafasi nyingi za kupata elimu ya juu ya masomo ya sayansi kama ya kwenye fani ya Madini.

“Sekta ya madini nchini Tanzania inaonyesha kuwa na mwanga mkubwa wa mafanikio kwa sasa na siku zijazo hivyo wakati ni huu wa kuchangamkia fursa hizi ili watanzania tuweze kunufaika nazo sambamba na kuwa na utaalamu wa kusimamia raslimali zetu”,alisisitiza.

Alisema atahakikisha kwamba atatumia fursa hiyo kupata na kusoma vizuri ili akirudi nyumbani aje kuitangaza vyema sekta ya madini na kuhakikisha kwamba anarudisha ujuzi na uelewa alioupata kwa maslahi ya sekta ya madini , kwa kampuni ya Barrick, jamii na Taifa kwa ujumla ili kuweka msingi mzuri wa maendeleo endelevu kwenye sekta hiyo na zingine mtambuka.

Akielezea historia fupi ya safari yake kielimu Riziki alisema alipata elimu yake ya msingi katika shule mbili tofauti hapo hapo Wilayani Mwanga , Shule ya Msingi, Mwanga na Kawawa na kuhitimu masomo yake mwaka 2017, elimu ya sekondari katika shule ya Mwanga na elimu ya sekondari ya juu katika Shule ya Sekondari ya Mkuu iliyopo Hai katika Mkoa wa Kilimanjaro.

“Nilichagua masomo ya sayansi (PCM) kwa sababu nilikuwa na ndoto ya kuwa mwanasayansi na kuhitimu mwaka 2024 nikiwa na daraja la kwanza kwenye masomo yangu,” alisema Mvungi.

Aliongeza kwamba baada ya ufaulu wa kidato cha tano na sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuamua kusomea masomo ya uhandisi wa madini na kwa muda mfupi chuo kile kimenifunza mengi pamoja na nidhamu , kujipambania , jinsi ya kuishi na watu nje na ndani ya masomo dira ambayo inamwongoza katika masomo yake katika Chuo Kikuu cha Johannesburg.

Riziki alisema aliamua kusomea uhandisi wa madini kwa sababu ni sekta pana na ya kimataifa na kujikita kwenye sekta hii kuna kunatoa fursa ya kutanua wigo wa uelewa na fikra chanya kwenye shughuli nzima za utafiti, uchimbaji na uchechuaji wa madini ya aina mbalimbali.

0/Post a Comment/Comments