SERIKALI KUWACHUNGUZA WAAJIRI WANAOTUMIA AKAUNTI ZA WATUMISHI KUOMBA MIKOPO

.........

Na Carlos Claudio, Dodoma

Serikali imeanza mchakato wa uchunguzi wa kubaini waajiri wanaotumia akaunti za watumishi wanaowasimamia kuomba mikopo binafsi bila ridhaa yao, huku ikionya kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, jijini Dodoma wakati Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ukiwajengea uwezo maafisa rasilimali watu na wahasibu kutoka wizara na taasisi za umma nchini.

Mkomi amesema serikali imeanza kufuatilia mnyororo mzima wa waajiri wanaojihusisha na vitendo hivyo, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuvunja sheria na taratibu za utumishi.

Amesema matumizi ya akaunti za watumishi kwa ajili ya mikopo binafsi bila ridhaa yao ni suala linalohitaji kuchukuliwa kwa uzito kutokana na madhara yanayoweza kuwapata watumishi husika.

Katika hatua nyingine, Mkomi ameitaka WCF kuangalia namna ya kupanua wigo wa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara mbalimbali wakiwa kazini, ikiwemo changamoto za kiafya kama shinikizo la damu.

Aidha, amewaonya waajiri wanaowatelekeza watumishi wanapokuwa hospitalini bila kuwasilisha taarifa katika maeneo husika, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watumishi wanapata msaada na stahiki zao kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema shughuli zinazotekelezwa na mfuko huo zinaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuhakikisha ustawi wa wananchi unakuwa jumuishi.

Amesema WCF inalenga kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara kutokana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi hawaachwi nyuma katika utekelezaji na kunufaika na matokeo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dkt. Mduma amesema WCF itaendelea kuhakikisha kunakuwa na ustawi, haki na usawa kwa wafanyakazi, akieleza kuwa misingi hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya 2050.

Amesema lengo ni kuhakikisha wafanyakazi wote wanaopata madhara yanayotokana na mazingira ya kazi wanapata haki na huduma stahiki, ili waweze kuendelea kunufaika na maendeleo yanayolengwa kupitia Dira hiyo.



 

0/Post a Comment/Comments