Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga na Lishe imeeleza kuwa inaendelea kuchunguza sababu zinazochangia kuendelea kwa tatizo la udumavu wa watoto nchini, licha ya baadhi ya mikoa kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula.
Takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa Iringa na Njombe ni miongoni mwa mikoa yenye viwango vya juu vya udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Akizungumza katika Wiki ya Chakula Duniani iliyoadhimishwa katika viwanja vya Usagara, mkoani Tanga, Ofisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga na Lishe, Peter Kaja, amesema udumavu ni kipimo kinachotumika kutathmini ukuaji wa mtoto kulingana na umri wake.
Amesema miaka mitano ya kwanza ya maisha ni muhimu katika ukuaji wa mtoto, hivyo lishe bora katika kipindi hicho inapaswa kupewa kipaumbele.
Amesema kipindi cha siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto kinahitaji uwekezaji mkubwa katika lishe, kuanzia wakati wa ujauzito hadi mtoto anapofikisha miaka miwili.
Hii ni kutokana na umuhimu wa lishe katika ukuaji wa mwili na ubongo wa mtoto, huku upungufu wa virutubishi muhimu ukiweza kuathiri ukuaji wake na uwezo wake wa kujifunza baadaye.
Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022, udumavu nchini ulikuwa asilimia 30.
Iringa ilikuwa na kiwango cha asilimia 56.9, huku Njombe ikiwa na asilimia 50.4, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto hiyo katika mikoa hiyo.
Kaja amesema Serikali imeongeza jitihada za kuboresha lishe kwa kuimarisha upatikanaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi, vikiwemo unga wa ugali, mafuta ya kula, chumvi na unga wa ngano.
Virutubishi vinavyotajwa kujumuishwa ni pamoja na asidi ya foliki, vitamini B12 na madini ya chuma, ambavyo vina umuhimu katika afya ya binadamu.





Post a Comment