Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge (IPU), Mhe. Mussa Azzan Zungu amewaasa Wajumbe kuhakikisha kuwa maazimio ya mkutano huo hayabaki kuwa maneno tu kwenye karatasi, badala yake wayapeleke katika mabunge yao ya kitaifa na kuyageuza kuwa sheria, sera na hatua madhubuti zinazoboresha maisha ya wananchi.
Mhe. Zungu amesema hayo wakati akitoa Hotuba ya kufunga Mkutano wa 153 leo Oktoba 9, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano cha Kimataifa Ausha (AICC) jijini Arusha.
“Kama nilivyosema wakati wa ufunguzi wa mkutano huu, tunawakilisha nchi, mifumo ya kisiasa, tamaduni na mitazamo tofauti. Hata hivyo, tunashiriki jukumu moja la pamoja la kuwahudumia wananchi wetu na kuchangia katika kuleta dunia yenye amani zaidi, haki na maendeleo endelevu,” amesema.
Amewaasa Wajumbe wa Mkutano hupo kuondoka Arusha wakiwa na dhamira mpya ya mazungumzo badala ya migawanyiko, ushirikiano badala ya migongano na ushirikishwaji badala ya kutengana katika makundi.
“Nguvu ya IPU inatokana na uwezo wetu wa kuungana licha ya tofauti zetu. Mikutano ya kimataifa lazima itusaidie kuielekeza dunia katika njia mpya, inayozingatia mazungumzo, utu, heshima, ushirikishwaji na mshikamano,” amesema.
Kwa upande mwingine Mhe. Zungu amempongeza Rais Mteule wa IPU, Mhe. Milton Dick, Spika wa Bunge wa Bunge la Wawakilishi la Australia aliyechaguliwa wakati wa Mkutano huo.
Mhe. Dick anachukua nafasi ya Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt Tulia Ackson ambaye anamaliza muda wake.
“Namtakia Rais Mteule kila la heri na tunatarajia kufanya kazi pamoja naye katika kujenga jumuiya ya kibunge imara na yenye ufanisi zaidi,” amesema.
Mhe. Zungu amemshukuru pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuandaa mkutano huo nchini.
“Namshukuru kwa uungaji mkono na mwongozo wake thabiti katika kuhakikisha tunakuwa na tukio lililoandaliwa vyema kwa ajili yetu sote,” amesema
Mhe. Zungu amewashukuru pia Watanzania wote hususan wakazi wa Arusha kwa kuwakaribisha wajumbe wote kwa uchangamfu na urafiki.
“Dunia imeshuhudia kuwa Tanzania ni nchi ya amani, umoja na ukarimu. Kwa kila mtu aliyefanya kazi nyuma ya pazia kufanikisha Mkutano huu, tunawashukuru,” amesema.
------------------------------------------











Post a Comment