Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuchochea ukuaji wa biashara za kilimo nchini kupitia uwezeshaji wa Kampuni ya Mboje Food Processor Company Limited ya Igunga, Tabora, inayojihusisha na uchakataji na uuzaji wa mchele.
Kupitia uwezeshaji huo, kampuni imeweza kununua na kusimika mashine za kisasa za kuchakata mpunga na kupanga madaraja, hatua iliyoongeza ufanisi na uwezo wa uzalishaji wa mchele.
TADB pia iliwezesha kampuni kupata gari kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa mizigo, pamoja na mtaji wa kununua malighafi na kukidhi mahitaji ya soko kwa wakati.
Matokeo ya uwezeshaji huo yameonekana katika ongezeko la ajira, ambapo wafanyakazi wa kudumu wameongezeka kutoka 13 hadi 23, huku ajira za msimu zikifikia takribani 150.
Kwa sasa, Mboje Food Processor ina uwezo wa kuchakata hadi tani 60 za mpunga kwa siku, huku ikijikita pia katika uchakataji wa mafuta ya alizeti na biashara ya mazao mchanganyiko.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joseph Shigela Mboja, anasema uwezeshaji wa TADB umefungua fursa zaidi za uzalishaji na masoko ndani na nje ya nchi, huku ukichangia kukuza mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.






Post a Comment