TANZANIA KUFUNGUA UBALOZI WAKE NCHINI ANGOLA - RAIS SAMIA


 ******

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza uamuzi wa Tanzania kufungua tena ubalozi wake nchini Angola, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Alhamisi, Oktoba 29, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, aliyeko nchini kwa ziara ya kitaifa.

Amesema amemuarifu Rais Lourenço kuhusu uamuzi huo na kwamba katika kipindi kijacho atateua balozi atakayesimamia shughuli za ubalozi na kuratibu ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Tanzania na Angola.

Rais Samia amebainisha kuwa uhusiano wa nchi hizo ulijengwa na viongozi waasisi, akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa kwanza wa Angola, Dkt. Agostinho Neto, wakati wa harakati za ukombozi wa Angola hadi ilipopata uhuru mwaka 1975.

Amesema viongozi waliofuata wameendeleza uhusiano huo hadi sasa, huku akimpongeza Rais Lourenço kwa juhudi zake za kukuza ushirikiano kati ya mataifa hayo.

Aidha, Rais Samia amesema ziara hiyo ni ya kwanza ya kitaifa kufanywa na Rais wa Angola nchini Tanzania kwa takribani miaka 47, tangu ziara ya Rais Agostinho Neto mwaka 1979.

Ameeleza matumaini yake kuwa kufunguliwa tena kwa ubalozi kutaimarisha mawasiliano na uratibu wa masuala ya pamoja, pamoja na kuweka msingi imara wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika nyanja mbalimbali za ushirikiano.

Hatua hiyo inatarajiwa kutoa msukumo mpya katika mahusiano ya kidiplomasia ya Tanzania na Angola na kuimarisha zaidi urafiki wa kihistoria uliodumu kwa miongo kadhaa.




0/Post a Comment/Comments