Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Tanzania itashirikiana na nchi wanachama wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOWCA) kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kitovu cha utaalamu wa usafiri wa majini.
Kihenzile ametoa kauli hiyo Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026, kuelekea mkutano wa 10 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la shirika hilo, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15 mwaka huu.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri wapatao 26 wanaosimamia uchukuzi na usafirishaji wa mizigo. Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Amesema ajenda kuu ni kuimarisha biashara baina ya nchi wanachama kupitia usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya maji.
Pia, mkutano huo utajadili namna ya kuboresha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi zisizo na mwambao wa bahari na zile zenye bandari.
Washiriki wengine wanatarajiwa kutoka taasisi za kikanda na kimataifa, zikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), AfCFTA, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC.
Akizungumzia umuhimu wa sekta hiyo, Kihenzile amesema usafiri wa majini una mchango mkubwa katika biashara ya kimataifa.
Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya Afrika husafirishwa kwa njia ya bahari, huku zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo ikitegemea usafiri huo.
Amesema ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika, kuna haja ya kuimarisha miundombinu inayounganisha bandari, reli, barabara, viwanda na masoko.
Kwa mujibu wa Kihenzile, Tanzania ina nafasi muhimu kutokana na eneo lake la kimkakati katika Bahari ya Hindi na ukanda wa Maziwa Makuu.
Ameitaja Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi jirani zisizo na mwambao wa bahari, zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika bandari na meli unapaswa kwenda sambamba na kuimarisha usalama wa majini, kulinda mazingira na kutumia teknolojia za kisasa.
Pia, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu ili sekta hiyo ichangie zaidi ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira.
Kihenzile amesema chuo hicho kitasaidia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, kukuza tafiti na ubunifu, pamoja na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya sekta ya usafiri wa majini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri wa Majini la Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOWCA), Kassim Mpaata, amesema gharama za ujenzi wa chuo hicho zitagawanywa kwa ushirikiano wa nchi wanachama, huku Tanzania ikiongoza mchakato huo.
Mpaata amesema mradi huo unalenga kuongeza fursa za mafunzo kwa vijana na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya usafiri wa majini.









Post a Comment