Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
DAR ES SALAAM: Tanzania imeanza kuchukua hatua za kuharakisha maandalizi ya Mkakati wa Muda Mrefu wa Maendeleo yenye Uzalishaji Mdogo wa Gesijoto (LT-LEDS), huku Serikali ikieleza umuhimu wa kupata rasilimali zaidi za kifedha na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.
Hatua hiyo imejadiliwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, pamoja na Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa, katika kikao na wawakilishi wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Mkutano huo ulifanyika jana, Oktoba 6, 2026, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, na ulihusisha majadiliano kuhusu namna ya kuharakisha maandalizi ya mkakati huo kupitia mpango wa Net-Zero Nature-Positive Accelerator.
Mpango huo unalenga kuunganisha juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na uhifadhi wa mazingira, bioanuai pamoja na maendeleo endelevu, kupitia Mradi wa Integrated Net-Zero Nature Positive Solutions for Climate Change and Biodiversity Protection, unaoratibiwa na TFS.
Akifungua kikao hicho, Mutasa alisema mazungumzo hayo yalilenga kuangalia namna Tanzania inaweza kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo ili kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani na kupata rasilimali zinazohitajika kukamilisha maandalizi na utekelezaji wa mkakati huo.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa mchakato huu unajenga uwezo wa ndani na unakuwa sehemu ya mipango yetu ya maendeleo, huku tukitumia fursa za ushirikiano na washirika wa maendeleo,” alisema.
Mtaalamu Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka GEF, Remy Ruay, alisema rasilimali zilizopo kwa baadhi ya shughuli za maandalizi hazitoshelezi mahitaji ya mchakato huo kutokana na kuhusisha sekta mbalimbali, mashauriano mapana ya wadau na ujenzi wa uwezo wa wataalamu.
Alisema takribani Dola 657,000 za Marekani zimetengwa kwa baadhi ya shughuli, wakati uzoefu wa nchi nyingine unaonyesha maandalizi ya mikakati ya muda mrefu yanaweza kugharimu kati ya Dola milioni moja na milioni 1.5.
“Modeli tunayotumia inapaswa kumilikiwa na nchi. Hatutaki kuwa na mfumo ambao wataalamu wa nje pekee ndio wanauelewa na kuutumia,” alisema Ruay, akisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania.
Majadiliano hayo yanafanyika wakati Tanzania ikiendelea kuoanisha maandalizi ya mkakati wa Net Zero na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC 3.0), ambao mpango wake wa utekelezaji na uwekezaji unaendelea kuandaliwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika kikao hicho, utekelezaji wa NDC 3.0 kwa kipindi cha miaka 10 unakadiriwa kuhitaji takribani Dola bilioni 8.6. Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NAP) pia umetajwa kuwa sehemu ya juhudi za Tanzania katika kuhamasisha rasilimali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika mjadala huo, Mhandisi Gertrude Lyatuu wa UNDP Tanzania, anayeshughulikia mazingira na mifumo ya ikolojia, pamoja na wataalamu wengine akiwamo Abbasi Kitogo, walisisitiza umuhimu wa kuunganisha sera za tabianchi, mazingira na maendeleo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Net Zero, Yusuph Tango, alisema utekelezaji wa baadhi ya shughuli tayari umeanza, ikiwamo maandalizi ya mkakati wa muda mrefu wa maendeleo ya nishati vijijini, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, nishati safi ya kupikia na uhamaji unaotumia nishati ya umeme..

Post a Comment