TRA YAKABIDHI KOMPYUTA 86 KWA TAASISI ZA SERIKALI KUIMARISHA HUDUMA KWA JAMII


 ******

SONGWE, Oktoba 30, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Songwe, imekabidhi kompyuta za mezani 86 na vifaa vyake kwa taasisi za serikali mkoani humo ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wa jamii katika ulipaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya Serikali yanayochangia maendeleo ya Taifa.

Taasisi zilizopokea vifaa hivyo ni Shule ya Sekondari Mlowo, Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Ileje, Jeshi la Polisi Wilaya ya Ileje, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe pamoja na Shule ya Sekondari Mpakani. Msaada huo unalenga kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kurahisisha utekelezaji wa majukumu katika taasisi hizo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa Ukaguzi na Ufuatiliaji wa TRA Mkoa wa Songwe, CPA Watson Mmasa, amesema msaada huo ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii unaolenga kurejesha kwa jamii kwa kutambua mchango wake kupitia ulipaji wa kodi. Ameongeza kuwa TRA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma na kuchangia maendeleo ya jamii.

Kwa upande wao, wawakilishi wa taasisi zilizopokea msaada huo wameishukuru TRA kwa kuzingatia mahitaji yao na kueleza kuwa kompyuta hizo zitasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku. Aidha, wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, pamoja na kujiepusha na vitendo vya magendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya Serikali na kuathiri maendeleo ya Taifa.

0/Post a Comment/Comments