********
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema limezindua kampeni maalumu ya msimu wa mwisho wa mwaka kwa wateja wa huduma ya Fiber Mlangoni Kwako, inayolenga kuwawezesha Watanzania kupata huduma za intaneti na mawasiliano kwa gharama nafuu.
TTCL imesema kupitia kampeni hiyo, wateja wapya na wa zamani watakaolipia kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi watanufaika na vifaa na huduma mbalimbali bila gharama za ziada.
Shirika hilo limeeleza kuwa ofa hiyo inajumuisha simu ya mezani, ruta (router), laini tatu za simu pamoja na huduma ya burudani ya T-Burudani.
Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, amesema kampeni hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kuendelea kuwasiliana na kutumia intaneti kwa urahisi, hususan katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mwita amesema huduma ya Fiber Mlangoni Kwako imekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka miwili, ikihudumia familia, wafanyabiashara wadogo na maeneo yenye shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesema TTCL inaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo XGPON, huku ikitekeleza awamu ya pili ya mradi wa Fiber Mlangoni Kwako katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Mwita amesema wateja watakaonufaika na ofa hiyo wanapaswa kufika katika ofisi au maduka ya TTCL yaliyo karibu nao wakiwa na namba zao za huduma (service number) ili kuhakikiwa na kupatiwa huduma zinazostahili.
Amesema huduma hiyo inapatikana katika maeneo yenye miundombinu ya TTCL, yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa na Unguja, Zanzibar, huku akiwahimiza Watanzania wanaoishi maeneo hayo kutembelea ofisi za shirika hilo kupata maelezo zaidi.










Post a Comment