TTCL YAWEKA MKAZO HUDUMA KWA MTEJA


*******

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeweka mkazo katika kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia na kuongeza ufanisi katika kushughulikia changamoto zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Mteja 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Anita Moshi, amesema mteja anapaswa kuwa kiini cha huduma zote za kampuni.

Moshi amesema maendeleo ya teknolojia yameongeza ushindani katika sekta ya mawasiliano, hivyo ubora wa huduma na uzoefu wa mteja ni muhimu kwa kampuni.

Amesema jukumu la kumhudumia mteja linawahusu wafanyakazi wote wa TTCL, bila kujali nafasi au idara wanayofanyia kazi.

Kwa mujibu wa Moshi, kaulimbiu ya mwaka huu ya “The Extra Mile” inalenga kuwafanya wafanyakazi kuchukua hatua kabla changamoto hazijawa malalamiko kutoka kwa wateja.

Amesema kampuni itaendelea kuboresha njia za kupokea maoni, kuongeza kasi ya kutatua changamoto na kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Moshi amesema TTCL pia itaendelea kuimarisha miundombinu yake, ikiwamo huduma ya Faiba Mlangoni Kwako, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha teknolojia bora na huduma bora.

Amewataka wafanyakazi kuwa mfano mzuri wa kampuni hiyo na kuhakikisha kila mteja anapata huduma inayokidhi matarajio, huku akiahidi kuwa TTCL itaendelea kusikiliza maoni ya wateja na kuboresha huduma zake.

























0/Post a Comment/Comments