Benki ya UBA Tanzania imezindua mfumo wa malipo wa Pan-African Payment and Settlement System (PAPSS), unaolenga kurahisisha miamala ya kuvuka mipaka kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wateja kutuma na kupokea fedha katika nchi za Afrika zinazoshiriki mfumo huo kwa kutumia sarafu za nchi zao.

“Huduma ya PAPSS kupitia WhatsApp na Facebook inalenga kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za kifedha, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya simu janja nchini Tanzania,” alisema Kalumwana.
Alifafanua kuwa huduma hiyo itawawezesha wateja kufanya miamala kupitia simu zao bila kulazimika kutembelea matawi ya benki. Kwa wateja wanaotembelea matawi, wanapaswa kuwa na taarifa za mpokeaji, ikiwemo namba ya akaunti na kiasi cha fedha wanachotaka kutuma.
Kalumwana alisema gharama za kutuma fedha kupitia PAPSS ni asilimia 2.5 ya kiasi kinachotumwa, huku tozo ya juu ikiwa dola 20 za Marekani, sawa na takribani Shilingi 70,000 za Tanzania.
Kuhusu vikomo vya miamala, alisema mteja anaweza kutuma hadi dola 5,000 kwa muamala mmoja na dola 10,000 kwa siku, kulingana na masharti ya huduma na kiwango cha ubadilishaji fedha cha siku husika.
Aliongeza kuwa mfumo huo unazingatia usalama wa miamala ya kifedha, huku benki kuu za nchi zinazoshiriki zikisimamia mifumo ya kifedha na viwango vya ubadilishaji fedha vinavyotumika. Pia, mtumaji anatakiwa kuwa na akaunti ya UBA, lakini mpokeaji anaweza kupokea fedha kupitia benki nyingine zinazoshiriki mfumo wa PAPSS bila kuwa na akaunti ya UBA.
Naye Geofrey Magugi, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa UBA Tanzania, alisema benki hiyo imekuwa ya kwanza nchini kuingia makubaliano na mfumo wa PAPSS kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za kifedha na kurahisisha biashara barani Afrika.
“Kujiunga na mfumo wa PAPSS ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za kifedha na kurahisisha malipo ya kuvuka mipaka, huku wafanyabiashara wakipata fursa ya kufanya miamala kwa urahisi zaidi katika nchi za Afrika zinazoshiriki mfumo huo,” alisema Magugi.



Post a Comment