VIJANA WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU KUJENGA FURSA KATIKA KILIMO


....

Vijana wametakiwa kutumia ipasavyo teknolojia, ubunifu na maarifa katika sekta ya kilimo ili kujenga fursa za ajira, biashara na kuongeza thamani ya mazao.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Kilimo, Gungu Mibavu, wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana la Kilimo Ikolojia Tanzania 2026.

Mibavu amesema kijana mwenye maarifa anahitaji mazingira ya kutumia maarifa hayo, huku mwenye bidhaa akihitaji soko na mwenye teknolojia akihitaji nafasi ya kutengeneza na kujaribu suluhisho linaloweza kujibu changamoto zilizopo katika jamii.

Amesema pia vijana wanaojihusisha na biashara wanahitaji mazingira wezeshi yatakayowasaidia kukuza shughuli zao na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi.

Aidha, amesema teknolojia za kidijitali, taarifa za masoko na mifumo mbalimbali ya usimamizi zinaendelea kubadilisha namna watu wanavyofanya biashara na kutafuta fursa, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia vijana.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kujiuliza kama teknolojia zinazotengenezwa zinaweza kutatua changamoto halisi zinazowakabili vijana na walengwa wengine, badala ya kuishia katika mipango na kauli zisizotekelezeka.

Amesema vijana wanapaswa kupewa nafasi katika maeneo yenye umuhimu kwa mustakabali wa kilimo na maendeleo ya taifa, huku wakipatiwa maarifa, teknolojia, mitaji na mazingira bora ya kukuza ubunifu na biashara zao.

 

0/Post a Comment/Comments