Wanasayansi nchini Tanzania wanachunguza teknolojia mpya ya kijenetiki inayolenga kuzuia mbu kusambaza malaria kwa binadamu.
Utafiti huo unafanywa na programu ya kimataifa ya Transmission Zero, inayolenga kuboresha mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Mkurugenzi wa programu hiyo katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk. Dickson Wilson Lwetoijera, amesema uelewa wa mazingira na tabia za mbu ni muhimu katika kudhibiti malaria.
Amesema mvua, halijoto, unyevunyevu na mabadiliko ya tabianchi huathiri mazalia ya mbu na kuenea kwa maambukizi.
Kupitia teknolojia hiyo, watafiti wanalenga kubadilisha vinasaba vya mbu ili kuzuia vimelea vya malaria kukua ndani yao na kupunguza uwezo wa kusambaza ugonjwa huo.
Dk. Lwetoijera amesema utafiti huo unafanyika hatua kwa hatua, huku athari zinazoweza kujitokeza kwa binadamu na mazingira zikifanyiwa tathmini. Kwa sasa, majaribio hayo yanafanyika katika maabara zenye udhibiti madhubuti nchini.
Programu hiyo inashirikisha IHI, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Imperial College London na Swiss Tropical and Public Health Institute. Hata hivyo, vyandarua vyenye dawa, tiba ya malaria na unyunyiziaji wa viuatilifu majumbani vinaendelea kuwa muhimu katika kudhibiti ugonjwa huo.

Post a Comment