BIHARAMULO
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, ambaye kwa sasa ni diwani wa Kata ya Nyanza, Leo Rushahu, amedondosha machozi mbele ya kikao cha madiwani wakati akiwatetea watumishi wa kituo cha afya Nyakanazi.
Hali hiyo imejitokeza wakati akiendelea kuchangia hoja ya upungufu wa watumishi kwenye kituo hicho cha afya, ambapo pamoja na mambo mengine amedai kinapokea wagonjwa wengi hadi usiku wa manane ukilinganisha na akidi ndogo ya watumishi waliopo.
Kutokana na wingi huo watumishi hao wamekuwa wakichoka sana na wakati mwingine kuwasilisha madai yao kwa baadhi ya viongozi kwa lengo la kunusuru maisha ya wagonjwa wanakuwa wamesongamana ukilinganisha na vituo vingine.
"Mimi mwenyewe huwa nakwenda kupata huduma za afya pale, unaweza kwenda saa tano usiku na ukashangaa kukuta idadi ya wagonjwa ilivyo kubwa, unaweza kufikiri ni asubuhi japo ni usiku, hivyo naomba kituo hicho kitazamwe kwa udharura wake" amesema Rushahu.
Licha ya kuwa siyo Diwani wa Kata hiyo, lakini ameonekana kuguswa na kadhia wanayopitia watumishi hao na kulishawishi Baraza kuongeza idadi ya watumishi kwenye kituo hicho hata kama itakuwa ni kupunguza kidogo kwenye baadhi ya vituo vya afya visivyokuwa na wagonjwa wengi.
Ameonyesha wasiwasi wake iwapo mvua zinazoendelea kuonyesha zitasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo yale ya mlipuko, na kwamba inaweza kusababisha majonzi makubwa kwa jamii kutokana na Idadi ya watumishi kushindwa kuhimili wingi wa wagonjwa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Innocent Mkandara, ameahidi kulishughulikia suala hilo huku akimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya hiyo kuona namna anavyoweza kutatua changamoto hiyo kutokana na udharura wake.
Kadhalika ameendelea kuwasisitiza madiwani kuendelea kushirikiana na wananchi wa maeneo yao kuanzisha ujenzi wa Zahanati kila Kijiji kama mwongozo wa serikali unavyoelekeza kwa lengo la wananchi kupata huduma hizo kwa umbali mfupi na kupunguza msongamano kwenye vituo vya afya.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Apolnary Mugarula, amezidi kukazia matumizi mazuri ya fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo vijijini ili ziwanufaisha wananchi na kutatua changamoto zinazo wakabili.
Katika hatua nyingine amesisitiza ukusanywaji wa fedha za mkopo usio na riba unaotolewa na halmashauri hiyo kupitia makundi ya Vijana, Wanawake na Makundi maalumu, ziweze kurejesha na kuwanufaisha wengine.




Post a Comment