HALMASHAURI ZATAKIWA KUONGEZA BAJETI KUREJESHA WANAFUNZI SHULENI

*******

Na Mwandishi Wetu

Halmashauri nchini zimetakiwa kuongeza juhudi za kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa sera ya kurejesha wanafunzi walioacha shule, ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. 

Wito huo umetolewa katika mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa halmashauri na wadau wa elimu kujadili utekelezaji wa sera hiyo.

Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Robert Mwendwa, amesema changamoto kubwa zinazokwamisha utekelezaji wa mpango huo ni ufinyu wa bajeti, uelewa mdogo wa jamii na miundombinu isiyokidhi mahitaji ya wanafunzi, hususan wasichana.

Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Robert Mwendwa, Akimzungumza kando mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa halmashauri na wadau wa elimu kujadili utekelezaji wa sera ya kurejesha wanafunzi walioacha shule, ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. 

Amesema halmashauri yake ina kata 21 na shule zilizotawanyika katika maeneo mbalimbali, hali inayofanya ufuatiliaji na uhamasishaji wa wanafunzi waliokatisha masomo kuwa mgumu. 

Ameongeza kuwa upungufu wa vyoo rafiki, maji na vyumba vya kujisitiri kwa wasichana ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi yao kuacha shule.

Mwendwa amesema halmashauri itaendelea kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, elimu kata, walimu wakuu na viongozi wa vijiji kuhamasisha familia kuhakikisha watoto waliokatisha masomo wanarejea shuleni. 

Pia, wataandaa mikutano kuelimisha jamii kuhusu sera na miongozo ya serikali.

Mwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Deogratias Temba,akimzungumza kando mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa halmashauri na wadau wa elimu kujadili utekelezaji wa sera ya kurejesha wanafunzi walioacha shule, ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. 

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Deogratias Temba, amesema mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka halmashauri 10 pamoja na wanajamii kutoka kata 12, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa Waraka Na. 2 wa Elimu wa mwaka 2021 na miongozo ya kurejesha wanafunzi shuleni. 

Amesema tathmini imebaini kuwa sera na miongozo ipo, lakini halmashauri nyingi hazina bajeti maalumu ya kugharamia utekelezaji wake.

Temba amesema hali hiyo inahitaji halmashauri kuweka mikakati ya kuingiza mahitaji ya kurejesha wanafunzi katika bajeti zijazo. 

Ameongeza kuwa elimu kwa jamii na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni ni muhimu katika kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo.

Afisa Mipango wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mwandishi Nchimbi, akimzungumza kando mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa halmashauri na wadau wa elimu kujadili utekelezaji wa sera ya kurejesha wanafunzi walioacha shule, ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. 

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mwandishi Nchimbi, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kutambua umuhimu wa kupanga bajeti inayozingatia mahitaji ya wanafunzi, hasa wasichana. Amesema halmashauri yake imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya miundombinu rafiki, taulo za kike na mipango ya kujenga mabweni ili kupunguza umbali wa wanafunzi kufika shuleni.

Ameongeza kuwa mila na desturi potofu zinazoathiri elimu ya mtoto wa kike zinapaswa kupigwa vita, huku jamii ikielimishwa kuhusu umuhimu wa kuweka shughuli za kimila katika vipindi visivyoathiri masomo. Amesisitiza kuwa watoto wanapaswa kupewa nafasi ya kuendelea na elimu bila vikwazo vinavyoweza kuzuilika.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Silvesta, akimzungumza kando mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa halmashauri na wadau wa elimu kujadili utekelezaji wa sera ya kurejesha wanafunzi walioacha shule, ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. 

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Silvesta, amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kuwarejesha baadhi ya wanafunzi, wakiwamo wasichana na wavulana, ingawa wengine wameshindwa kuendelea kutokana na changamoto za kiuchumi, ukosefu wa walezi, mimba na ndoa za utotoni.

Silvesta amesema hatua inayofuata ni kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia kuhusu umuhimu wa kurejesha watoto shuleni, kuimarisha malezi chanya na kuhamasisha uanzishwaji wa vituo vya kulelea watoto wadogo wakati wa mchana. Amesema ushirikiano wa familia, halmashauri na jamii ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu na nafasi ya kutimiza ndoto zao.

Kwa ujumla, washiriki wamekubaliana kuwa mafanikio ya kurejesha wanafunzi shuleni yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya halmashauri, serikali, wazazi na jamii kwa ujumla. Wamesisitiza kuwa uwepo wa sera na miongozo pekee hautoshi bila kutengwa kwa bajeti, kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kuondolewa kwa vikwazo vinavyowafanya watoto kukatisha masomo.



















0/Post a Comment/Comments