JENGO LA TAWIRI KUCHOCHEA UHIFADHI WA KISAYANSI

........

Na Mwandishi Wetu, Arusha 

BODI  ya Udhamini ya Mfuko wa Wanyamapori Tanzania (TWPF), imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). 

Pongezi hizo zinetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TWPF,  Prof. Jafari Kideghesho, kwenye ziara iliyofanywa na wajumbe wa Bodi hiyo kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la kisasa jijini Arusha, huku akiitaka TAWIRI kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.

Prof. Kideghesho, amesema ujenzi wa jengo hilo ni jitihada za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuendelea kuimarisha uhifadhi endelevu wa wanyamapori kwa maslahi mapana ya taifa hivyo ni vyema likakamilika kwa wakati uliopangwa. 

Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora amesema ni moja ya mikakati ya Wizara hiyo ya kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori unaoongozwa na mbinu za kisayansi.

Dkt. Lobora ameongeza kuwa, Wizara kupitia Idara anayoiongoza itaendelea kusimamia kikamilifu maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo kama ilivyoelekezwa na Bodi hiyo. 

"Kwa niaba ya uongozi wa Wizara yetu, natoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndie Mhifadhi namba moja, kwa kuridhia sehemu ya fedha za Mfuko wa TWPF  na Hazina kutumika katika ujenzi wa jengo hili litakalokuwa na ofisi na maabara ya kisasa," alisema Dkt. Lobora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Eblate Mjingo, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo, akisema jengo hilo litakuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha tafiti zenye tija kwa uhifadhi na utalii endelevu.

Ujenzi wa jengo hilo la ghorofa tatu, unaoendelea katika eneo la Njiro, Arusha, umefikia asilimia 41 na unatarajiwa kugharimu Sh. bilioni 8.9 hadi kukamilika kwake.





0/Post a Comment/Comments