KUPATA HUDUMA ZA AFYA HAIPASWI KUTEGEMEA KIPATO, MAKAZI WALA HADHI YA MTU - RAIS SAMIA

Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na viongozi mbalimbali, wadau wa masuala ya Afya kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Kisayansi kuhusu Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Novemba, 2026.
....

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema upatikanaji wa huduma bora za afya haupaswi kutegemea kipato, mahali anapoishi mtu wala hadhi yake katika jamii, akisisitiza umuhimu wa usawa katika utoaji wa huduma hizo.

Amesema kila mwanamke na mtoto anapaswa kupata huduma kulingana na mahitaji yake, hususan wanaoishi katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa huduma za afya.

Rais Samia ameyasema hayo leo Alhamisi, Novemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe.

Akisisitiza hoja hiyo, Rais Samia amenukuu kauli ya mwanazuoni na tabibu wa afya ya jamii, Dk. Paul Farmer, aliyesema kuwa wazo la baadhi ya maisha kuwa na thamani ndogo kuliko mengine ndilo chanzo cha mambo mengi yasiyo sawa duniani.

Amesema ujumbe huo unapaswa kuwa msingi wa utekelezaji wa huduma za afya kwa kuhakikisha hakuna mwananchi anayenyimwa huduma bora kutokana na hali yake ya kiuchumi au mazingira anayoishi.

Rais Samia amewataka Serikali, wataalamu wa afya, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi za kiraia kutumia utaalamu, maarifa na rasilimali walizonazo kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa usawa.

Amesema ugharamiaji endelevu, ubunifu katika kutatua changamoto na mifumo imara ya afya ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma hiyo.

0/Post a Comment/Comments