Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa, Ethiopia
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo, jijini Addis Ababa, Ethiopia, kwa lengo la kujadili fursa za kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ethiopia.
Mhe. Londo aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, pamoja na ujumbe wa maafisa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, mara baada ya kushiriki katika Mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika uliofanyika nchini Ethiopia.
Akizungumza katika mazungumzo hayo, Mhe. Londo amesema ni muhimu kwa Tanzania kutumia fursa za biashara za kikanda na kimataifa pamoja na ushirikiano na wadau wa maendeleo, wakiwemo TradeMark Africa, katika kuimarisha mifumo ya biashara, kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua wigo wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, huku biashara ikiwa miongoni mwa nyenzo muhimu za kufikia malengo hayo.
Ameongeza kuwa hadi Juni 2026, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa zenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 19.98, akibainisha kuwa kipaumbele cha Serikali ni kuongeza kiwango na thamani ya bidhaa hizo, ikiwemo kutumia fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo, amemshukuru Naibu Waziri Londo na ujumbe wake kwa kuiwakilisha vema Tanzania na kupeperusha bendera ya nchi katika mkutano huo, akieleza kuwa ushiriki huo ni muhimu katika kuitangaza Tanzania na kufungua fursa za biashara na uwekezaji katika soko la Ethiopia na nchi nyingine za Afrika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Londo alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Ushirika wa Uganda, Mhe. Sanjay Tenna, ambapo walijadili namna ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Uganda, pamoja na kuongeza fursa za masoko kwa bidhaa za nchi hizo mbili.
Aidha, alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Utalii wa Burundi, Christine Niragira, kwa lengo la kuongeza fursa za biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Burundi.
Katika mazungumzo hayo, walijadili pia umuhimu wa kuimarisha miundombinu inayorahisisha biashara, hususan Bandari ya Kigoma na maeneo yanayounganisha Tanzania na nchi jirani, ili kuongeza mauzo ya bidhaa katika masoko ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Uganda.
Akitoa mfano wa fursa zilizopo katika soko la Burundi, Mhe. Londo amesema nchi hiyo iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.31, lakini Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 134 pekee, hali inayoonesha uwezekano mkubwa wa kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko hilo.




Post a Comment