MAKUMBUSHO YA TAIFA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA AKIOLOJIA UDSM

..............

Makumbusho ya Taifa la Tanzania yachangia kuimarisha uelewa kuhusu chimbuko la binadamu na umuhimu wa uhifadhi wa urithi wa akiolojia kupitia maonesho ya vielelezo halisi yaliyofanyika leo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Leo, tarehe 27 Novemba, yamefanyika maadhimisho ya miaka 40 ya Akiolojia Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Maadhimisho haya yamefunguliwa na Mgeni Rasmi, Bwana Emmanuel Makota, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Teknolojia kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, aliyemwakilisha Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Makumbusho ya Taifa imewakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Noel Biseko Lwoga, aliyeshiriki katika maadhimisho hayo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kukuza elimu, tafiti za akiolojia na uhifadhi wa urithi wa Taifa.

Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu “ *Four Decades of Archaeology Education and Research: Heritage Preservation, Tourism and National Development,”* inayosisitiza mchango wa akiolojia katika utafiti,uhifadhi wa urithi, utalii na maendeleo ya Taifa.

Katika maadhimisho hayo, Makumbusho ya Taifa iliweka onesho maalumu la vielelezo halisi vya akiolojia vinavyofadhiwa katika taasisi hiyo, vikiwemo mafuvu ya zamadamu wa kale na zana za mawe vinavyotoa ushahidi kuhusu historia ya binadamu na jamii za kale.

Kupitia onesho hilo, wanafunzi na watafiti wamepata fursa ya kujifunza moja kwa moja kuhusu chimbuko la binadamu na kutambua thamani ya urithi wa akiolojia katika kuelewa historia ya Taifa na dunia.

Ushiriki huo umeimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kuongeza fursa za kujifunza kwa vitendo, huku ukiendelea kutangaza umuhimu wa mikusanyo ya Makumbusho katika kuhifadhi na kurithisha urithi wa Taifa kwa vizazi vijavyo.










 

0/Post a Comment/Comments