MALIASILI, JESHI LA POLISI WATOA MAFUNZO KWA WAMILIKI WA HUDUMA ZA MALAZI KUELEKEA AFCON 2027

...........

Na Jackson Joseph Nyasebwa, Arusha

WIZARA ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini imetoa mafunzo kwa wamiliki wa huduma za malazi kuhusu; usalama, utoaji wa huduma bora kwa wateja, kufuata sheria pamoja na namna ya kujisajili katika programu tumizi iitwayo Destination Tanzania katika kipindi hiki ambacho Tanzania iko katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika  (AFCON) yatakayo fanyika kuanzia mwezi Juni, 2027 kwa ushirikiano na nchi za, Kenya na Uganda.

Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, kambi za kitalii na vituo vingine vya malazi kuelewa na kuzingatia taratibu za kiusalama katika utoaji wa huduma kwa wageni watakaotembelea nchini wakati wa michuano hiyo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Dainess Kunzugala, ameeleza kuwa maandalizi ya AFCON 2027 yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kupokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Bi. Dainess Kunzugala, amesema kuwa huduma za malazi ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa utalii, hivyo ni muhimu kuhakikisha watoa huduma wanazingatia viwango vinavyotakiwa katika masuala ya usalama, usafi, maadili ya huduma bora kwa wateja na utoaji wa taarifa sahihi kwa wageni.

"Wamiliki wa huduma za malazi wote katika Mkoa wa Arusha wanapaswa kuwa tayari kutoa huduma zitakazowafanya wageni watakao kuja wakati wa mashindano ya AFCON 2027 kuwa na kumbukumbu ya kudumu na kuwa na shauku ya kurudi tena baada ya mashindao kuisha,” amesema, Bi. Kunzugala.

Mafunzo hayo kwa watoa huduma za malazi katika Mkoa wa Arusha yamefanyika leo katika ukumbi wa Chuo cha Fedha Arusha (IAA) na kuhudhuriwa na wamiliki wa huduma za malazi yaani AirBnB, Homestays, Hoteli, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na Jeshi la Polisi Tanzania. 

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027, anayehusika na malazi, usafiri na ufasiri wa lugha, Bw. Allen Alex, amebainisha kuwa wageni wapatao milioni 1.8 wanatazamiwa kuja Afrika Mashari kushiriki mashindano ya AFCON 2027 na angalau watu laki 5 mpaka 6 wataweka makazi yao nchini Tanzania. Hivyo wamiliki wa huduma za malazi wanapaswa kuwa tayari kuwakarimu wageni hao ili waweze kuwa na kumbukumbu ya kudumu kuhusu Tanzania.

“Ninyi watoa huduma za malazi ndio ambao mtasababisha wageni waiseme Tanzania vizuri au vibaya, waendelee kuwepo na kutamani kurudi au wasirudi. Wageni wataamua hayo kutokana na namna mtakavyowahudumia na ukarimu wenu kwao,” amesisitiza Bw. Alex.

Naye Mkuu wa Dawati la Utalii na Diplomasia la Jeshi la Polisi Tanzania, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), WJ Tenga, amesema ni muhimu kwa watoa huduma za malazi kuweka namba muhimu za dharura katika maeneo ya shughuli zao ili mteja aweze kuripoti  jambo ambalo anaona linahitaji msaada wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto au huduma ya dharura ya kimatibabu ili kujenga imani kwa watalii na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii wa Kimataifa.

“Tunapoelekea kwenye haya mashindano ya AFCON 2027 maeneo yote ya huduma za malazi ni vizuri mkaweka namba za watoa huduma mnaoshirikiana nao kama bodaboda na magari ya kukodi, pia muwashauri wageni wakati gani ni sahihi  kutumia bodaboda au gari hii itaongeza thamani ya huduma mnayotoa,” amesema Bw. Tenga.

Bw. Tenga  amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa elimu ya usalama wa wageni na mali zao, utambuzi na utoaji wa taarifa za matukio ya kiusalama, udhibiti wa vitendo vya uhalifu pamoja na namna ya kushirikiana na vyombo vya usalama katika maeneo yanayotoa huduma za malazi nchini.

Mafunzo hayo kwa watoa huduma za malazi ni moja ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukamilisha maandalizi ya kupokea wageni watakaohudhuria mashindano ya AFCON 2027, huku ikilenga kutumia mashindano hiyo kutangaza vivutio vya utalii, kuongeza idadi ya watalii na kukuza mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini.









 

0/Post a Comment/Comments