Na Jackson Joseph Nyasebwa – DAR ES SALAAM
WIZARA ya Maliasili na Utalii imewataka wamiliki wote na waendeshaji wa nyumba za malazi zinazotangazwa kupitia mfumo wa Airbnb na Homestay kuhakikisha wanarasimisha huduma hizo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sekta ya Utalii nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na wamiliki na waendeshaji wa huduma za malazi AirBnB na Homestays, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utali katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Richie Wandwi amesema, urasimishaji wa huduma za malazi kupitia mifumo ya kidijitali unafanyika katika mazingira yanayotambulika kisheria, yanayozingatia viwango vya ubora, usalama wa wageni na taratibu za usimamizi wa Sekta ya Utalii.
“Biashara zote hizi tunazozifanya katika utalii, tunazifanya kwa mujibu wa Sheria ya Utalii na kanuni zake, kwa hiyo wadau wa sehemu anayolala mtalii ni moja ya kivutio cha utalii hivyo inaratibiwa kwa sheria, sera na kanuni za utalii ambazo ni vitu muhimu kwa watoa huduma za malazi kuzizingatia,” amesisitiza Bw. Wandwi
Bw. Wandwi, amebainisha kuwa, Tanzania inapoelekea kwenye mashindano ya AFCON 2027 kurasimisha huduma za malazi za AirBnB na Homestay kutasaidia kuwa na takwimu sahihi za watoa huduma za malazi, uwezo wa utoaji huduma, pamoja na kuhakikisha watoa huduma wanawajibika katika utoaji wa huduma bora kwa watalii wa ndani na nje ya nchi, kuongeza uwazi katika biashara ya malazi, kuimarisha ushindani na kuongeza machango za Sekta ya Malazi katika Uchumi wa Taifa.
Sekta ya Utalii nchini ni moja ya nguzo za kiuchumi ikichangia asilimia 25 ya mauzo ya kigeni, huku ikichangia asilimia 17.2 katika Pato Ghafi la Taifa (GDP) na kutoa ajira milioni 3.7 kwa Watanzania, lengo likiwa ni kufikia idadi ya watalii milioni 8 ifikapo Mwaka 2030.
Kwa upande wake Afisa Sheria katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Shafii Rugine, ameeleza kuwa baadhi ya watoa huduma za malazi wanakabiliwa na changamoto ya kutokidhi matakwa ya kisheria, hatua inayoweza kuathiri taswira ya Tanzania kama nchi inayotoa huduma bora na salama za utalii na kwamba ni wakati muafaka kwa wamiliki kufanya maboresho na kujisajili ili kukidhi matakwa ya kisheria.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Utalii, Sura ya 65, huduma za malazi ni miongoni mwa shughuli zinazopaswa kusajiliwa na kupata leseni zinazotambulika kisheria. Matakwa hayo yanahusu pia nyumba za wageni (AirBnB, Homestays) na fleti zinazotumika kwa ajili ya malazi ya watalii, kwa kufanya hivyo mmiliki anakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa huduma pasipo usumbufu,” alisema Bw. Rugine.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa agizo hilo unafanikiwa, Wizara imehimiza ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na wamiliki wa nyumba hizo ili kuongeza uelewa kuhusu taratibu za usajili, utoaji wa leseni, viwango vya ubora na usalama wa wageni.







Post a Comment