MARS COMMUNICATIONS YAAHIDI KUWAFIKIA WATEJA NCHI NZIMA

...

Na Carlos Claudio, Dodoma

Kampuni ya Mars Communications Ltd imewashukuru wateja wake kwa kuendelea kuiunga mkono, ikisema ushirikiano wao umeiwezesha kampuni hiyo kuendelea kukua na kudumu katika soko la Tanzania.

Shukrani hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo nchini (Country Marketing Director), Bw. Mustafa Bhalloo, wakati wa maonyesho ya teknolojia ya madini na ukandarasi ya MAT Builders and Contractors Global.


Bw. Bhalloo amesema wateja ni nguzo muhimu katika mafanikio ya kampuni hiyo, akieleza kuwa haiwezi kufikia malengo yake bila ushirikiano na uaminifu wao.


Amesema Mars Communications inajihusisha na usambazaji wa bidhaa za Hisense, Samsung na LG, zikiwemo simu za mkononi, televisheni, friji, mashine za kufulia na kukaushia nguo pamoja na viyoyozi (AC).


Amebainisha kuwa katika kipindi hiki cha joto, kampuni imejikita zaidi katika kuwapatia wananchi viyoyozi vya aina mbalimbali, ikiwemo vyenye bei nafuu, ili kuwawezesha kupata unafuu na kukabiliana na joto.


Aidha, amesema bidhaa zinazouzwa na kampuni hiyo zina ubora na uimara, akieleza kuwa baadhi ya bidhaa zimeendelea kufanya kazi kwa zaidi ya miaka nane hadi 10 tangu ziliponunuliwa.


Bw. Bhalloo amesema kampuni hiyo imeendelea kupanua huduma zake kwa kuwafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Lushoto, Nzega, Kahama na Geita.


Ameongeza kuwa Mars Communications ina maduka makuu ya bidhaa (flagship stores) katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Zanzibar, ambayo yana bidhaa mbalimbali za Hisense na Samsung, yakiwa na mpangilio wa kisasa unaokidhi viwango vya kimataifa.


Amesema kampuni imeendelea kuzingatia uwezo wa Watanzania kwa kuweka bei zinazoweza kumudu, huku pia ikitoa huduma ya ununuzi wa simu na bidhaa nyingine kwa mkopo kwa wateja wanaokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa.


Bw. Bhalloo amewahimiza wananchi kutembelea maduka ya Mars Communications Ltd ili kujionea na kununua bidhaa mbalimbali, huku akiwashukuru kwa kuendelea kuunga mkono bidhaa za Hisense na kampuni hiyo kwa ujumla.
 

0/Post a Comment/Comments