MBARAWA AWATAKA WAMILIKI WA MABASI KUHAKIKISHA USALAMA KUELEKEA SIKUKUU

******

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wamiliki wa mabasi na vyombo vingine vya usafiri kufanya ukaguzi wa kina ili kuhakikisha usalama wa abiria wakati wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Profesa Mbarawa alisema ongezeko la safari katika kipindi cha sikukuu linahitaji maandalizi na tahadhari zaidi ili kuzuia ajali.

Alikuwa akimwakilisha Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, katika ufunguzi wa maadhimisho ya pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu, yaliyohusisha pia utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika sekta hiyo.

Alisisitiza madereva kuzingatia sheria za barabarani na kuepuka mwendo kasi pamoja na vitendo vingine vinavyoweza kuhatarisha maisha ya abiria.

Aidha, aliwataka abiria kutokuwa watazamaji wanapobaini ukiukwaji wa sheria, bali kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu mwenendo hatarishi wa madereva.

Profesa Mbarawa alisema usalama wa maisha unapaswa kupewa kipaumbele kuliko kuwahi kufika katika safari, akiwataka madereva kuendesha kwa uangalifu.

Alisisitiza kuwa ni bora abiria kuchelewa kufika wanakokwenda kuliko kuhatarisha maisha kwa sababu ya mwendo kasi.









0/Post a Comment/Comments