Na Carlos Claudio, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Pascal Chinyele, ametembelea maonyesho ya teknolojia ya madini na ukandarasi ya MAT Builders and Contractors Global na kuwahimiza Watanzania kutumia fursa kama hizo kujionea teknolojia zinazoweza kurahisisha shughuli zao za uzalishaji.
Mhe. Chinyele amesema amefarijika kupata fursa ya kutembelea mabanda hayo, huku akivutiwa zaidi na mitambo ya kuchimba na kuchenjua madini.
Amesema mitambo hiyo inaweza kuleta mabadiliko makubwa wakati nchi ikiwa na ajenda kubwa ya utafutaji na uchimbaji wa madini.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo inaendana na sera ya Serikali, ambapo madini yanaelekea kuwa chanzo kikubwa cha mapato na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi.
Ameshauri wachimbaji wa kati kuangalia namna ya kupata mitambo hiyo. Pia aliwataka wachimbaji wadogo kufikiria kuungana na kuinunua, ili kuachana na vifaa duni vya asili vinavyohitaji matumizi makubwa ya nguvu.
Katika ziara hiyo, Mbunge huyo amevutiwa pia na mashine ya kuchakata uwele, zao linalostahimili ukame na kustawi katika maeneo yenye mvua haba kama Dodoma.
“Zamani sisi Wagogo tulikuwa tunatumia fimbo kuchapa ule uwele mpaka ukae vizuri, lakini sasa ziko mashine ambazo bei zake sio mbaya,” alisema.
Amesema ameambiwa kuwa mojawapo ya mashine hizo inauzwa Shilingi milioni 6.5. Alishauri wakulima wenye uwezo mdogo waungane, akitoa mfano wa watu sita wanaoweza kuchangia kila mmoja Shilingi milioni moja na kidogo.
Amewahimiza wananchi wasikate tamaa ya kulima uwele kwa sababu ya ukosefu wa miti ya kuupigia, kwa kuwa mashine zipo. Alisema zao hilo linaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wananchi.
Mhe. Chinyele pia alijionea majiko yanayotumia umeme kidogo. Alisema ameelezwa kuwa uniti za umeme za Shilingi 2,000 zinaweza kutosheleza mahitaji ya kupika kwa siku nzima.
Aidha, ametaja mashine za kukamua alizeti, karanga na mazao mengine, pamoja na mashine za kuchanganya saruji na mchanga kwa ajili ya kutengeneza matofali. Alisema zipo zinazotumia mafuta na pia zinazotumia umeme kupitia mota.
Katika mabanda hayo kuna pia bidhaa mbalimbali za wajasiriamali wadogo, ikiwemo asali ya nyuki wakubwa na wadogo.
“Karibuni sana ndugu zangu wa Tanzania, karibuni wakazi wa Dodoma kwa ajili ya kujipatia bidhaa mbalimbali ambazo zinapatikana karibu na nyumba,” alisema Mhe. Chinyele.


Post a Comment