#Amshukuru Mhe. Dkt. Samia kwa Imani Aliyompatia Kuongoza TARURA
Dodoma
Mtendaji Mkuu aliyemaliza muda wake wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amewaasa viongozi na watumishi wa taasisi hiyo kudumisha umoja, mshikamano na mahusiano mazuri huku akiwataka kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanakuwa fursa ya kuimarisha taasisi badala ya kurudisha nyuma mafanikio yaliyokwisha kupatikana
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuitumikia TARURA kwa kipindi chote cha Utumishi wake
Mhandisi Seff ametoa rai hiyo wakati akitoa ujumbe wake wa kuwaaga watumishi wa TARURA baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka tisa cha kuiongoza taasisi hiyo akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazuri yaliyofanyika, kuboresha maeneo yanayohitaji maboresho na kuzingatia mifumo, taratibu na misingi ya utendaji wa taasisi.
Amesema mabadiliko ya uongozi ni sehemu ya kawaida ya ukuaji wa taasisi hivyo watumishi wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha Mtendaji Mkuu mpya kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyofikiwa yanakuwa msingi wa kupiga hatua kubwa zaidi.
Ameongeza kuwa anaamini TARURA ina uwezo mkubwa wa kuendelea kukua na kutoa huduma bora zaidi kwa watanzania akiwataka watumishi kutopima mafanikio ya kiongozi kwa muda aliokaa madarakani bali kwa ubora wa taasisi anayoiacha, watumishi aliowajenga na mabadiliko chanya aliyosaidia kuyafanikisha.
Akizungumzia safari yake ya uongozi, Mhandisi Seff amesema anaondoka TARURA akiwa na hazina kubwa ya uzoefu, urafiki, mafunzo na mahusiano aliyoyajenga katika kipindi chote cha miaka tisa huku akitoa shukrani kwa watumishi na wadau wote waliokuwa sehemu ya safari yake.
Amesema anathamini mchango wa kila mmoja aliyemsaidia, kumshauri, kumkosoa kwa nia njema na kumtia moyo akibainisha kuwa licha ya kutofautiana katika baadhi ya mambo wote walikuwa na dhamira moja ya kujenga na kuendeleza taasisi.
Katika ujumbe wake wa mwisho kwa familia ya TARURA, Mhandisi Seff amewaachia watumishi mambo sita muhimu aliyojifunza katika kipindi chake cha utumishi akiyataja kuwa ni uadilifu katika utendaji, kutambua kuwa uongozi ni dhamana na si umiliki pamoja na kuwaheshimu watu wote kwa kutambua kuwa kila mtumishi ana mchango wake katika mafanikio ya taasisi.
Mengine ni kujenga umoja na ushirikiano akisisitiza kuwa taasisi haiwezi kusonga mbele ikiwa kila mmoja atatanguliza maslahi binafsi, kuwekeza katika maarifa na kuwaandaa watumishi wa kizazi kijacho na mwisho ni kutanguliza wananchi katika kila jambo kwa kutambua kuwa uwepo wa TARURA una maana kubwa kutokana na huduma inayowapatia wananchi.
Amesisitiza kuwa umoja, uadilifu, kujifunza na kumweka mwananchi mbele vinapaswa kuendelea kuwa nguzo muhimu ya utendaji wa TARURA ili kuhakikisha taasisi hiyo inazidi kuimarika na kutimiza dhamira yake ya kutoa huduma bora za barabara za vijijini na mijini nchini.










Post a Comment