MKURUGENZI SIDO AWATAKA WANUFAIKA WA TUINUKE PAMOJA KUBORESHA BIDHAA KUSHINDANA MASOKONI

...............

Na Carlos Claudio, Dodoma

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), CPA Ahmed Kitara, amewataka wajasiriamali wanufaika wa Mradi wa Tuinuke Pamoja kuendelea kuboresha bidhaa zao kwa kuzingatia ubora, vifungashio na mahitaji ya soko ili kuongeza ushindani na kunufaika na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.

CPA Kitara ametoa wito huo Novemba 3, 2026 jijini Dodoma, alipotembelea banda la wanufaika wa Mradi wa Tuinuke Pamoja katika Maonesho ya Viwanda na Biashara yanayoelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda na Sera ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2025, unaotarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026.

Mradi wa Tuinuke Pamoja unatekelezwa na Shirika la Aga Khan Foundation katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, ukiwa na lengo la kuwawezesha wajasiriamali kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha.

Amesema bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali waliopatiwa mafunzo kupitia SIDO zimeonesha ubora na uwezo wa kushindana katika masoko mbalimbali, akibainisha kuwa baadhi ya bidhaa hizo zinazalishwa na vijana, hususan wanawake.

Aidha, amewashauri wajasiriamali kujisajili na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kupata uthibitisho wa ubora pamoja na nembo ya Made in Tanzania, hatua itakayoongeza thamani na kuimarisha ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya ndani na kimataifa.

Amesisitiza kuwa SIDO itaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia maeneo manne muhimu ambayo ni mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji, teknolojia rahisi za uzalishaji, huduma za mitaji pamoja na upatikanaji wa maeneo ya kufanyia kazi.

Amewahimiza vijana na wajasiriamali kutumia fursa hizo kuanzisha na kuendeleza biashara zao kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora zinazokidhi mahitaji ya walaji na ushindani wa soko.

Akizungumza katika maonesho hayo, mnufaika wa Mradi wa Tuinuke Pamoja kutoka Kata ya Chang’ombe, Wilaya ya Dodoma, Keto Khalfan, amesema maelekezo waliyopata kuhusu ubora, ufungashaji na usajili wa bidhaa yatawasaidia kuboresha uzalishaji na kupanua wigo wa masoko yao.

Amesema kwa sasa bidhaa zao zinauzwa zaidi ndani ya Mkoa wa Dodoma na baadhi ya mikoa jirani, huku akieleza kuwa SIDO imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kupitia mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji, usimamizi wa fedha na ufungashaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Haruna Makunda, mnufaika wa mradi huo kutoka Kikundi cha Kondoa Women Group, Wilaya ya Kondoa, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umewawezesha kupata elimu muhimu kuhusu usajili wa biashara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa kupitia TBS.

Amesema elimu hiyo itawawezesha kuboresha vifungashio na viwango vya bidhaa zao ili kukidhi mahitaji ya soko la kisasa na kupata fursa ya kuingia katika masoko mapana zaidi, ikiwemo soko la kimataifa.

Naye mjasiriamali kutoka Kikundi cha Girls Power, Esther Kakurwa, Wilaya ya Chamwino, amelipongeza Shirika la Aga Khan Foundation kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja kwa kuwashirikisha wajasiriamali katika maonesho hayo, akisema yamewapa fursa ya kutangaza bidhaa zao, kujifunza na kupata uelewa wa namna bora ya kukuza biashara.

Amehimiza wajasiriamali wengine kujitokeza kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kibiashara ili kujitangaza, kujenga mahusiano na wadau wa biashara pamoja na kutafuta masoko mapya yatakayochochea ukuaji wa biashara zao.




 

0/Post a Comment/Comments