Kampeni ya "Na Sisi Tupo" imeanza kuwafikia wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati, ikilenga kuwapa vijana elimu kuhusu Virusi vya UKIMWI, hasa vijana wenye ulemavu, ili washiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, wakati wa midahalo ya vijana kupitia mradi wa My Data Our Health iliyofanyika katika Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI).
Kampeni hiyo inatekelezwa na FDH kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS). Salali amesema lengo ni kupunguza maambukizi mapya na kujenga taifa lenye vijana walio salama, wenye uelewa na wanaoweza kuepuka madhara ya ugonjwa huu.
Amesema watu wenye ulemavu ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.
Mojawapo ya sababu ni mitazamo hasi katika jamii, ikiwemo dhana potofu kwamba kuwa na uhusiano na mtu mwenye ulemavu kunaweza kumwondolea mtu maambukizi ya VVU. Dhana hiyo huwafanya baadhi ya watu kuingia kwenye mahusiano yasiyo na nia njema na watu wenye ulemavu.
Salali ametoa mfano wa watu viziwi, akisema ili wapate elimu sahihi kuhusu kujikinga, ni lazima ujumbe uwafikie kupitia lugha yao ya alama. "Tuna wajibu wa kuhakikisha elimu hii inawafikia kwa njia wanazoweza kuzielewa," alieleza.
Ameongeza kuwa vita dhidi ya UKIMWI haiwezi kupiganwa na taasisi moja.
Inahitaji ushirikiano wa wadau wote katika kuongeza uelewa, kuhamasisha matumizi ya njia salama za kujikinga na kuipa jamii elimu ya kukabiliana na ugonjwa huu.
Amewataka wanafunzi kutumia elimu yao kufikisha ujumbe mbali zaidi, hasa kwa wenzao wenye ulemavu. "Mtu mwenye ulemavu ni binadamu kama binadamu wengine, na anastahili kupata elimu ya kutosha kuhusu njia za kujikinga," alisisitiza.
Salali amesema FDH ina miradi katika mikoa 25 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, na kampeni ya "Na Sisi Tupo" itaendelea kuwafikia vijana katika maeneo hayo.
Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Disemba 1, yatakayofanyika jijini Dodoma, wanafunzi na vijana wote wamealikwa kushiriki shughuli mbalimbali, ikiwemo mbio za jogging na midahalo kuhusu VVU na hatua za kuchukua.
Na Carlos Claudio, Dodoma.


Post a Comment