SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kukatika kwa huduma ya umeme katika mikoa ya Mbeya na Songwe baada ya nguzo za kusafirisha umeme kuanguka katika eneo la Inyala, mkoani Mbeya.
Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa Novemba 21, 2026, imeeleza kuwa tukio hilo limehusisha nguzo ya njia mpya ya kusafirisha umeme ya kilovoti 400 inayotekelezwa kupitia Mradi wa TAZA.
Pia, nguzo za njia ya umeme wa kilovoti 220 inayounganisha Iringa na Mbeya zimeathirika.
TANESCO imesema wataalamu wake tayari wamewasili eneo la tukio na wanaendelea na kazi ya kurekebisha miundombinu iliyoharibika.
Hata hivyo, shirika hilo limeonya kuwa kurejea kwa huduma kunaweza kuchukua muda kutokana na ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na kuanguka kwa nguzo hizo.
TANESCO imewahakikishia wananchi kuwa inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa taarifa zaidi kadiri kazi za ukarabati zitakavyoendelea.
Wakazi wa Mbeya na Songwe wametakiwa kuwa na subira wakati jitihada za kurejesha huduma ya umeme zikiendelea.

Post a Comment