OTR YAFUNGUA MILANGO KWA RMB KUSHIRIKI MAGEUZI YA TAASISI ZA UMMA


 *****

Na Mwandishi wa OTR

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imefungua milango kwa Benki ya Rand Merchant (RMB) kubaini fursa za ufadhili na uwekezaji katika taasisi za umma zilizo katika usimamizi wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati na kuimarisha uwezo wa kifedha wa kampuni hizo.

Mwaliko huo ulitolewa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipokutana na ujumbe wa benki hiyo, ulioongozwa na Bw. John Njuguna, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wateja wa Taasisi katika Ukanda wa Afrika Mashariki, katika ofisi za OTR jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalihusu fursa za ufadhili katika sekta za miundombinu, nishati jadidifu, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, madini, dawa na maeneo mengine ya uzalishaji. 

Lengo lilikuwa kuangalia namna utaalamu wa kifedha wa RMB unavyoweza kusaidia taasisi na kampuni za umma kupata mitaji ya kutekeleza miradi na kupanua shughuli zao.

Bw. Mchechu alisema OTR iko tayari kuratibu ushirikiano kati ya benki hiyo na taasisi za umma ili kubaini miradi yenye tija kibiashara na kuandaa mifumo ya ufadhili inayokidhi mahitaji ya kila taasisi.

OTR inasimamia taasisi na kampuni za umma 308, zikiwemo kampuni 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki hisa chache. 

Thamani ya jumla ya uwekezaji katika taasisi na kampuni hizo inafikia Sh trilioni 92.3, ikiwa ni mtaji mkubwa wa umma ambao unaweza kutumika zaidi kuchochea shughuli za kiuchumi na ukuaji wa uchumi nchini.

Bw. Mchechu alisema Serikali inazihimiza taasisi za umma kuimarisha uwezo wao wa kujiendesha kifedha kwa kutumia ipasavyo rasilimali na mali walizonazo ili kuvutia mitaji, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa fedha zinazotengwa katika bajeti ya Serikali.

Alieleza kuwa njia mbadala za kupata mitaji ni pamoja na mikopo kutoka benki za biashara, utoaji wa hati fungani na uuzaji wa hisa kupitia soko la mitaji.

Aliihimiza RMB kuchunguza fursa zilizopo katika taasisi hizo na kuandaa mapendekezo ya ufadhili yatakayojadiliwa kwa pamoja na OTR na kampuni husika.

Kwa upande wake, Bw. Njuguna alisema RMB ina nia ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma nchini, ikitumia uzoefu wake katika kufadhili miradi ya miundombinu na shughuli za kibiashara katika masoko mbalimbali ya Afrika.

Alibainisha kuwa vipaumbele vya Tanzania katika maendeleo ya miundombinu, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika biashara na usafirishaji wa kikanda, vinatoa fursa kwa benki hiyo kuchangia kupitia suluhisho za kifedha na uwekezaji zinazolingana na mahitaji ya miradi husika.

Naye Mkuu wa Suluhisho za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu wa RMB kwa Afrika, Bi. Sindisiwe Mosoeu, alieleza kuhusu mifumo mbalimbali ya ufadhili inayoweza kutumika katika miradi ya taasisi za umma.

Mifumo hiyo ni pamoja na ufadhili wa miradi, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, na ufadhili wa miradi ya nishati jadidifu.

Alieleza kuwa aina ya ufadhili inayofaa kwa kila mradi itategemeana na aina ya shughuli zinazotekelezwa, uwezo wa mradi kuzalisha mapato, uwezekano wake wa kujiendesha kibiashara na uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje.

Bi. Mosoeu pia alieleza kuhusu uzoefu wa RMB katika kufadhili miradi ya nishati jadidifu, hususan inayotumia nishati ya jua, upepo na maji katika nchi mbalimbali za Afrika. 

Uzoefu huo unaweza kuwa na manufaa kwa taasisi za umma zinazolenga kuendeleza miradi ya nishati na kupanua vyanzo vyao vya mitaji.

Mtaalamu wa Uandaaji wa Miundo ya Uwekezaji katika Masoko ya Kimataifa wa RMB kwa Afrika, Bw. Sinethemba Mvandamba, alisema benki hiyo ina uwezo wa kuwaunganisha wateja wake na vyanzo vya mitaji katika masoko ya kimataifa, hatua inayoweza kupanua wigo wa chaguzi za ufadhili zinazopatikana kwa kampuni na taasisi barani Afrika.







0/Post a Comment/Comments