RC SENYAMULE: HAKUNA MWENYE KIBALI CHA KUKATISHA UHAI WA MWENZAKE, ULEVI USIWE KISINGIZIO

.........

Na Carlos Claudio Mpwapwa,

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wananchi kuacha tabia ya kukatisha uhai wa wenzao na wa kwao wenyewe, akisisitiza kuwa hakuna mtu mwenye kibali cha kuchukua uhai wa mwingine, hata kama amefanyiwa jambo kubwa kiasi gani.

Ametoa kauli hiyo katika kijiji cha Nzase, Wilaya ya Mpwapwa, alipofanya mkutano wa hadhara na kusikiliza kero za wananchi, baada ya kutembelea miradi ya maendeleo ya Serikali katika eneo hilo.

Senyamule amesema Serikali inataka kuchukua hatua za kuzuia vifo kabla havijatokea badala ya kuchukua hatua baada ya madhara, kwa kuwa waliopoteza maisha hawawezi kurudishwa. Aliwataka wazazi na viongozi kuwakemea na kuwaonya vijana na watoto, huku wakifundishwa kuwa ubinadamu ni kuhimili changamoto kubwa za maisha.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya matukio ya mauaji yanatokana na ulevi. "Unywaji haukatazwi, lakini ulevi ni kunywa zaidi ya kipimo unachoweza kuhimili, na akili inakuhama hadi unaona hata kuua ni jambo dogo," alisema.


 Ameongeza kuwa mhusika hushtuka pombe ikiisha, akiwa tayari ametenda kosa litakalomweka gerezani kwa miaka mingi.

Kutokana na hali hiyo, ameagiza watendaji wa vijiji na kata kusimamia kikamilifu muda wa kufungua na kufunga vilabu vya pombe kwa mujibu wa sheria za Serikali.

Kuhusu msongo wa madeni, Senyamule amewataka wananchi kutokimbia vikwazo kwa kujiua au kuua wengine, akitolea mfano mtu aliyejinyonga mjini Dodoma kwa kudaiwa shilingi 700,000. "Maisha ni mapambano. Waliofanikiwa hawakufanikiwa kirahisi, walivuka vikwazo vingi," alisema.

Amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ina utashi mkubwa wa kudumisha amani na utulivu mkoani Dodoma, na kwamba yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya kukatisha uhai atachukuliwa hatua kali za kisheria.


 

0/Post a Comment/Comments