TAKUKURU TEMEKE YAONGEZA MAPATO YA HALMASHAURI KWA SH1.17 BILIONI, YABAINI CHANGAMOTO MIRADI YA SH13.24 BILIONI


 ******

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikisha kuongeza mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa Sh1.17 bilioni, huku ikibaini changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya Sh13.24 bilioni katika Manispaa za Temeke na Kigamboni.

Mafanikio hayo ya ukusanyaji wa mapato yametokana na ufuatiliaji wa ulipaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) pamoja na usimamizi wa utozaji wa faini kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Akizungumza Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TAKUKURU kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Emma Mwasyoge, amesema hatua hizo zililenga kuongeza mapato ya Serikali na kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa fedha za umma.

Mwasyoge amesema katika ufuatiliaji wa ushuru wa huduma, kampuni 94 zilifikiwa na kufanyiwa uhakiki wa malipo kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo kampuni 50 zilibainika kuwa na madeni au kulipa pungufu ya ushuru huo.

Amesema baada ya kampuni hizo kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua stahiki, zililipa jumla ya Sh1,066,020,516.90.

Aidha, amesema kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jumla ya Sh104.6 milioni zilikusanywa kutokana na utozaji wa faini kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa, yakiwemo Tandika, Mbagala, Kongowe na Buza.

Katika hatua nyingine, Mwasyoge amesema TAKUKURU ilifuatilia miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya Sh13.24 bilioni, ambapo ilibaini changamoto mbalimbali zilizohusisha ucheleweshaji wa kuanza kwa miradi, vifaa kutofikishwa kwa wakati, kuchelewa kukamilika kwa kazi pamoja na baadhi ya wakandarasi kutokuwa na usajili kutoka mamlaka husika, ikiwemo OSHA na Bodi ya Wakandarasi.

Amesema kati ya miradi hiyo, mitatu yenye thamani ya Sh12,239,354,234 inatekelezwa katika Manispaa ya Temeke, huku miwili yenye thamani ya Sh1,001,500,000 ikitekelezwa katika Manispaa ya Kigamboni.

Ameongeza kuwa katika ukaguzi huo pia ilibainika baadhi ya miradi kutumia matofali yasiyokidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Hata hivyo, amesema baada ya kubaini changamoto hizo, TAKUKURU ilitoa maelekezo kwa wahusika ili kuhakikisha kasoro hizo zinarekebishwa ndani ya muda uliowekwa.

Amesema wakandarasi waliagizwa kukamilisha taratibu za usajili katika mamlaka husika, vifaa vilivyokuwa vimechelewa vilifikishwa katika maeneo ya miradi, huku matofali yasiyokidhi viwango yakiondolewa na kubadilishwa na yale yenye ubora unaotakiwa.

Baadhi ya miradi iliyotajwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Tungi awamu ya pili wenye thamani ya Sh710 milioni, ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Tundwi Songani, Shule Mpya ya Msingi Sakafu Tano Mwembe Bamia pamoja na Shule Mpya ya Msingi ya English Medium Vigoa, Sakafu Tano.

Mwasyoge amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za TAKUKURU katika kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia viwango, sheria na taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya TAKUKURU na mamlaka za Serikali za Mitaa ni muhimu katika kudhibiti vitendo vya rushwa, kuimarisha usimamizi wa mapato na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili kupitia rasilimali za umma.


0/Post a Comment/Comments