TGNP YAWAWEZESHA WADAU KULINDA HAKI YA WASICHANA KUPATA ELIMU



NA MWANDISHI WETU

Wawakilishi wa vituo vya Taarifa na Maarifa katika kata 14 za halmashauri saba zinazotekeleza mradi wa kuwawezesha wasichana kurejea shuleni, wamepatiwa mafunzo kuhusu masuala ya jinsia na haki ya kupata elimu.

Mafunzo hayo yamefanyika leo, Novemba 18, 2026, katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea washiriki uwezo wa kuwasaidia wasichana waliokatiza masomo kurejea shuleni.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Deogratias Temba, amesema mradi huo unalenga kulinda haki za wasichana na kuwawezesha waliokatiza masomo kutokana na ujauzito kurejea shuleni kwa mujibu wa mwongozo wa serikali.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Deogratias Temba,Akimzungumza na washiriki.

Amesema washiriki wanapaswa kutumia elimu watakayoipata kuelimisha jamii kuhusu haki za wasichana, kuzuia mimba za utotoni na kuweka mikakati ya kuwawezesha waliokatiza masomo kurejea shuleni.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Deogratias Temba,Akiedelea kuwafundisha washiriki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mandawa, Halima Saidi Liba, amesema atatumia elimu hiyo kuwafikia wanafunzi, wazazi na walimu ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa wasichana kuendelea na masomo.

Amesema pia atahamasisha viongozi wa kata kutenga bajeti kwa ajili ya kuwasaidia wasichana waliokatiza masomo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na wadau.


Katibu wa kikundi cha Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) kutoka Kata ya Suruke, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, Khadija Ali Salum, Akimzungumza akichangia mada katika mafunzo hayo.

Naye Katibu wa kikundi cha Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) kutoka Kata ya Suruke, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, Khadija Ali Salum, amesema mafunzo hayo yatamwezesha kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu madhara ya mimba za utotoni.

Khadija amesema atatembelea shule mbalimbali kuwahamasisha wanafunzi kujiepusha na mimba za utotoni na kuendelea na masomo yao.

Amesema pia atatoa hamasa kwa wasichana waliopata ujauzito kutokata tamaa, bali kutumia fursa zilizopo kurejea shuleni na kuendelea na elimu.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanalenga kuwawezesha wawakilishi hao kutumia vituo vya Taarifa na Maarifa kuelimisha jamii na kuweka mikakati ya kuhakikisha wasichana waliokatiza masomo wanarejea shuleni.














0/Post a Comment/Comments