Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa ukwepaji kodi ili kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki katika soko na kulinda wafanyabiashara wanaotekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa uaminifu na kwa hiari.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Kitengo cha Intelijensia ya Kodi jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu Mwenda amesema ni muhimu kuimarisha mifumo ya utambuzi na udhibiti wa vitendo vya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza kuwa, wafanyabiashara wanaokwepa kodi wamekuwa wakufanya biashara kwa gharama zisizo sawa na wale wanaolipa kodi stahiki, hali inayoweza kuvuruga ushindani wa haki na kuwakatisha tamaa walipakodi waaminifu.
Aidha, amesisitiza kuwa TRA itaendelea kuchukua hatua za kuboresha utendaji wa Kitengo cha Intelijensia ya Kodi kwa kutumia taarifa na mbinu mbalimbali za kiuchunguzi katika kubaini na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amehimiza walipakodi wote kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kulipa kodi kwa usahihi na kwa wakati, na kuwashukuru Walipakodi wote kote nchini ambao wamekuwa wakitekeleza wajibu wa kulipa kodi kwa hiari.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu amesema wanaendelea kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kurahisisha huduma za kodi na kuwawezesha walipakodi kutekeleza wajibu wao kwa urahisi, haraka na kwa ufanisi zaidi.
Amesema matumizi ya teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa walipakodi, kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika michakato ya kikodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Amesisitiza kuwa TRA itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma za kodi zinapatikana kwa urahisi, zinakuwa rafiki kwa watumiaji na kupunguza muda na gharama ambazo walipakodi hutumia kutekeleza wajibu wao wa kikodi.
Aidha, ameitaka Idara ya TEHAMA kuendelea kubuni na kuboresha mifumo inayokidhi mahitaji ya walipakodi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa imara, salama na yenye ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Bw. Emmanuel Nko amesema wataendelea kuimarisha mifumo ya IDRAS na TANCIS ili iendelee kuwa na ufanisi katika utoaji huduma za kodi.
Wakati huo huo Bw. Mwenda ameahidi kuwa TRA itaendelea kutoa huduma bora za Kodi kwa walipakodi kwa nchi nzima ili kuwezesha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.
Amesema dhamira ya TRA ni kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za Kodi kwa nchi nzima na kuahidi kuwa pamoja na kuwapatia huduma hizo bora wataendelea kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
Kamishna Mkuu amewashukuru Walipakodi wote kwa nchi nzima kwa kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati na kuwaeleza kuwa TRA ipo tayari kuwahudumia muda wote.
Aidha amewapongeza watumishi wa TRA kwa nchi nzima kwa kuendelea kuwahudumia walipakodi na kuwezesha biashara zao wakitambua kuwa bila Walipakodi hakuna TRA.
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Kinondoni Bw. Azizi Rajab Soka amesema wapo tayari kuendelea kutoa huduma bora kwa walipakodi kwa kuwasikiliza na kuwezesha biashara zao.
Mwisho



Post a Comment