WATAALAM WA M&E MALIASILI NA UTALII WAIBUKIA NGORONGORO

.............

Na Mwandishi Wetu, Arusha 

TIMU ya Wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake, wamefanya utalii katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kama sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani. 

Akiongoza msafara huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Bure Nassibu amesema pamoja na Kikao Kazi cha maafisa hao, safari hiyo ni fursa kwao ya kutembelea vivutio vya utalii nchini na kuhamasisha wananchi kufanya utalii wa ndani. 

Ameongeza kuwa anaushukuru uongozi wa Wizara kwa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na kuwapatia fursa wataalamu hao ya kukutana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya Ufuatiliaji na Tathmini katika mazingira tulivu ambayo yanapatikana katika hifadhi za maliasili zilizopo chini ya Wizara. 

Hatua hiyo imetoa nafasi kwa wataalam hao kujifunza na pia kuhamasisha utalii wa ndani kupitia ziara kama hiyo.  

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Shirika la Makumbusho ya Taifa Bw. James Mganga,  pamoja na kuipongeza Wizara kwa maono hayo, amesema kuwa kwao kama washiriki imekuwa ni nafasi adhimu kwa kuwa imewapa mawanda mapanda ya uelewa juu ya uhifadhi na utekelezaji wa kazi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara hiyo katika kuendeleza uhifadhi endelevu wa maliasili na kukuza Sekta ya Utalii kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Wataalamu hao wapo mkoani Arusha kwa Kikao Kazi cha maandalizi ya Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E Framework) utakaowezesha kazi za Ufuatiliaji na Tathmini kufanyika kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyopangwa na Wizara hiyo yanafikiwa na kuleta matokeo yanayotarajiwa.




 

0/Post a Comment/Comments